Rais Magufuli azindua viwanda.

RAIS John Magufuli amezindua viwanda vikubwa vitatu na mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu, na ulazaji wa mabomba makuu kutoka Mlandizi hadi Dar es Salaam, katika siku ya pili ya ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, kwanza, Rais Magufuli amezindua kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Tanzania Ltd ,kilichopo katika eneo la viwanda Kibaha ambacho kina uwezo wa kutengeneza mifuko ya sandarusi 53,000 ,kwa siku kwa ajili ya kuhifadhia mazao.

Aidha, Dk Magufuli amezindua mradi wa kutengeneza matrekta 2,400 aina ya Ursus ambao utagharimu Sh bilioni 55, na matrekta hayo yatasambazwa nchi nzima kwa ajili ya kuboresha sekta ya kilimo.

Dk Magufuli ametoa mwito kwa wamiliki wa viwanda hivyo kujali maslahi na usalama wa wafanyakazi waliowaajiri, amezitaka benki nchini kujielekeza kufanya biashara na wananchi kwa kuwakopesha mitaji wafanyabiashara na wajasiriamali badala ya kutaka kufanya biashara na serikali na ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha viwanda vya chuma vinatumia malighafi za hapa nchini kutoka Mchuchuma na Liganga.

Leo Rais Magufuli atakamilisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani kwa kuzindua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona Drink Ltd, kuzindua kiwanda cha kukausha matunda cha Elven Agric Company na kuzindua mradi wa barabara ya Bagamoyo – Msata.

 

 

 

 

Exit mobile version