Kaimu Rais wa Nigeria amesema kuwa Rais Muhammadu Buhari anatarajiwa kurejea nyumbani katika muda mfupi ujao baada ya kuwa jijini London, Uingereza kwa zaidi ya miezi miwili kwa ajili ya matibabu wakati wasiwasi ukizidi kuhusu afya yake.
Makamu wa Rais Yemi Osinbajo amezungumza na waandishi wa habari jana, siku moja baada ya kukutana na Buhari.
Osinbajo amesema Buhari alikuwa katika hali nzuri na anaendelea kupata nafuu haraka. Alisema walizungumza kwa karibu saa moja.
Osinbajo hakutoa maelezo mengine kuhusu afya ya Buhari aliye na umri wa miaka 74, ambaye aliondoka Nigeria kwenda London mnamo Mei 7.
Buhari pia amemaliza karibu wiki saba mjini London mapema mwaka huu, kutokana na matatizo ya kiafya na kisha baadaye akasema hakuwahi kuwa mgonjwa kiasi hicho maishani mwake.
