Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa na mkutano wa pili na Rais wa Urusi Vladimir Putin wakati wa mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi la G20 uliofanyika Ujerumani mwezi huu, ambao awali haukuwekwa wazi.
Viongozi hao wawili walikutana rasmi kwa mara ya kwanza kwa mazungumzo ya masaa mawili Julai 7 mbele ya vyombo vya habari vya dunia.
Baadaye Trump alisema Putin alikanusha madai kwamba Urusi iliingilia kati uchaguzi wa rais wa Marekani wa mwaka 2016.
Katika mazungumzo yao ya pili ambayo hayakuwekwa wazi awali, Trump na Putin walizungumza kwa zaidi ya saa moja nzima wakiwa pamoja na mkalimani wa Putin.
Mbali na kuwepo kwa wasiwasi kwamba Urusi ilihusika katika kumuweka madarakani Trump, Ian Bremmer, Rais wa Kundi la kimataifa la ushauri wa kisiasa, Eurasia, ameliambia gazeti la Marekani la The Hill kwamba Trump kushiriki mazungumzo hayo bila ya kuwepo mkalimani wake ni kukiuka itifaki ya usalama wa kitaifa.
