Rais wa muda wa mrefu wa Gambia Yahya Jammeh aliiba kiasi dola milioni 50 za taifa hilo kabla kukimbilia uhamishoni nchini Guinea ya Ikweta Janauri mwaka huu baada ya kuiongoza nchi hiyo kwa miaka 22.
Hayo ni kwa mujibu wa waziri wa sheria wa Gambia Abubacarr Tambadou.
Waziri Tambadou amesema Jammeh binafsi aliamuru fedha kutolewa kutoka kwa benki kuu ya Gambia na benki ya Gamtel kati ya 2013 na 2017.
Waziri huyo aidha amesema wamepata kibali cha mahakama kuzifungia au kuzizuia kwa muda mali zinazofahamika kumilikiwa na rais wa zamani Jammeh pamoja na kampuni zinazohusishwa moja kwa moja na kiongozi huyo.
Waziri Tambadou amesema amri ya mahakama iliyotolewa hapo jana inalenga kumzuia Jammeh kuziuza mali zake na amethibitisha amri hiyo inahusu tu mali za kiongozi huyo nchini Gambia pekee.
