Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amewafuta kazi Majaji 14 waliokuwa wanagoma kwa muda wa miezi miwili sasa.
Kiir ametangaza hatua hiyo kupitia redio ya taifa, na kuwaambia raia wa Sudan Kusini kuwa Majaji hao wamefutwa kazi.
Inaaminiwa kuwa hatua hii imechukuliwa baada ya mgomo huo kukwamisha shughuli za Mahakama hiyo hasa jijini Juba.
Majaji hao wamekuwa wakigoma kushinikiza nyongeza ya mshahara lakini pia, kutaka kufutwa kazi kwa Jaji Mkuu Chan Reec Madut.
Madut amekuwa akishtumiwa na Majaji hao kwa kushindwa kuwatetea kuongezwa mshahara.
Mgomo huo ulimfanya rais Kiir kuunda Kamati ya kuchunguza kiini cha mgomo huo na mwezi uliopita, iliwasilisha ripoti yake kwa rais Kiir.
Hata kabla ya kufutwa kazi, Majaji hao waliamua kutorudi kazini hadi pale matakwa yao yangetekelezwa.
