Kiongozi wa upinzani aliyeko uhamishoni Riek Machar ametoa wito wa kuanza upya mazungumzo ya amani nje ya taifa linalokumbwa na vita la Sudan Kusini.
Machar ametoa taarifa hiyo hapo jana kupitia mpatanishi wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa, ambapo pia alikataa kukemea machafuko yanayoendelea nchini humo au kutangaza usitishwaji wa mapigano kutoka upande wake.
Hii imetokea wakati Marekani ikiwaonya viongozi nchini Sudan Kusini kuwa wako katika hatari ya kupoteza msaada wa Marekani kama watakataa kushiriki katika mazungumzo ya amani na kuheshimu muda uliowekwa wa kusitishwa mapigano.
Maelfu ya watu wameuawa na zaidi ya milioni 3.5 wamekimbia makazi yao baada ya Rais Salva Kiir kumtuhumu aliyekuwa naibu wake Machar kwa kupanga njama ya mapinduzi.
