Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, SACP Fortunatus Musilimu amefanya ziara ya kushtukiza Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mikoani na Nchi jirani, Ubungo na kuzindua uwekaji wa namba za simu kwenye mabasi kwa ajili ya abiria kutoa taarifa pale madereva wanapokiuka sheria za Usalama barabarani.
Kamanda Musilimu ameeleza kuwa hatua hiyo ni kusaidia abiria kutoa taarifa pindi madereva wanapokiuka sheria za Usalama Barabarani na kuhatarisha maisha yao, na kusema zoezi hilo ni la nchi nzima ambalo litakuwa endelevu na ukaguzi wa mara kwa mara utafanyika kuhakikisha namba hizo hazitolewi kwenye mabasi hayo.
Lakini pia Kamanda Musilimu ametoa onyo kali kwa madereva na makondakta watakao ziondoa namba hizo katika mabasi, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na kuwaasa kuziacha namba hizo katika mabasi yao ili wasafiri waweze kuzitumia.
