Saudi Arabia kusitisha kununua silaha kutoka Ujerumani na kansela Angel Merkel atoa wito Ghuba kuacha mashambulizi ya anga nchini Yemen.

Saudi Arabia inasema haitaki tena kununua silaha kutoka Ujerumani, kauli inayokuja wakati Kansela Angela Merkel akitoa wito kwa taifa hilo kubwa la Ghuba kuacha mashambulizi ya anga nchini Yemen.

Kansela Merkel aliwasili jana nchini Saudi Arabia kwa ziara ya kikazi. Naibu Waziri wa Uchumi wa Saudia, Mohammed al-Tuwaijiri, ameliambia jarida la “Der Spiegel” la hapa Ujerumani kwamba sasa nchi yake itajizuwia kuomba silaha zaidi kutoka Ujerumani, na badala yake kujielekeza kwenye ushirikiano wa kiuchumi na sekta nyengine.

Al-Tuwaijiri amesema kuwa Saudia inayafahamu mazingira ya kisiasa yalivyo na haitaki kusababisha matatizo zaidi kwa serikali ya Ujerumani, akisisitiza kuwa Ujerumani na Saudia zina mambo mengine muhimu zaidi kuliko silaha.

Akiwa na ujumbe mkubwa wa wafanyabiashara, Kansela Merkel alipokewa na kufanya mazungumzo na Mfalme Salman na warithi wake hapo jana, ikiwa ziara yake ya kwanza baada ya miaka saba nchini Saudia.

Exit mobile version