Serikali imesisitiza kuwa sera ya Afya ya mwaka 2007 inaeleza kuwa huduma za kina mama wajawazito katika vituo vya ngazi zote zinatakiwa kutolewa bila malipo.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto,Dk.Khamis Kigwangala,wakati akijibu swali la mbunge wa Viti Maalum, Manira Musta Khatibu,aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kufuta tozo na gharama za vifaa vya kujifungulia na upasuaji kama ilivyofuta za matibabu ya wazee na wagonjwa wa kisukari.
Dk.Kigwangala amesema serikali haijawai kuweka tozo na gharama za vifaa vya kujifungulia na upasuaji.Amesema huduma hizo zinatolewa katika ngazi zote katika vituo vya Umma vya kutolea huduma kwa gharama za serikali.
Hata hivyo amesema ili kuhakikisha sera hiyo inatekelezwa kwa vitendo,wizara inahakikisha akina mama wanakuwa na vifaa muhimu vya kujifungulia, ambapo vifuko maalum vyenye vifaa vya kujifungulia kwa wanawake 500,000 vitasamazwa nchi nzima kulingana na uhitaji.
Katika hatua nyingine Dk.Kigwangala amesema kuwa kutokana na sera ya afya kwa sasa serikali imejikita zaidi katika kuimalisha sekta ya afya.
