SERIKALI imetangaza rasmi kugawa pembejeo za korosho bure kuanzia Msimu wa Kilimo wa 2017/2018, ambapo wakulima sasa wapata bure pembejeo aina ya salfa zilizokuwa zikiuzwa kwa bei ya ruzuku.
Kauli hiyo ya Serikali ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ,alipokuwa anafungua mkutano wa kila mwaka wa wadau wa korosho uliofanyika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Mipango, mjini Dodoma.
Alisema nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha vikwazo vyote vilivyokuwa vinawakabili wakulima wa zao hilo vinaondolewa ili kuwawezesha kupata tija zaidi kutokana na zao lao.
Alisema lengo la Serikali ni kuona mashamba yaliyotelekezwa na yenye mikorosho iliyozeeka yanafufuliwa ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa wakulima na nchi kujipatia kipato cha kutosha.
Awali akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Nchini (CBT), Anna Abdallah, alisema bodi hiyo imenunua tani 18,000 za pembejeo, aina ya Salfa ambayo inatumika kudhibiti na kutibu ugonjwa wa ubwiriunga unaowasumbua wakulima wa zao hilo.
Amesema kiasi hicho ni sawa na asilimia 95 ya pembejeo zote zilizoagizwa kwa msimu huu wa kilimo, ambapo pembejeo nyingine ni pamoja na dawa za maji za kunyunyizia na mabomba ya kupulizia na jumla ya Sh bilioni 43.5 zitatumika katika kununua, kusambaza na malipo ya mawakala
