SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2017 wenye marekebisho ya sheria 15 ikiwamo Sheria ya Ushuru wa Bidhaa.
Kwa mujibu wa marekebisho hayo, ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji baridi umeongezeka kutoka Sh 58 kwa lita hadi Sh 61 ikiwa ni sawa na ongezeko la shilingi tatu.
Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti imepinga ongezeko hilo la shilingi tatu kwenye vinywaji baridi ikisema hatua hiyo itazorotesha ukuaji wa viwanda nchini.
Akiwasilisha Muswada huo jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema sheria hizo zinahusu masuala ya fedha, kodi, ushuru, tozo, na mawasiliano ili kupunguza, kurekebisha, au kufuta viwango vya kodi, ushuru, ada na tozo mbalimbali ili kuboresha ukusanyaji wa kodi.
Dk Mpango amesema marekebisho hayo yamezingatia mkakati wa taifa wa kukuza uchumi wa viwanda, na kwamba kiwango cha ushuru kwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini kimepunguzwa au kubakia ilivyo sasa.
Mengine aliyozungumzia ni ongezeko la ushuru katika mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa Sh 40, Sheria ya Benki Kuu inayorekebishwa ili kuweka sharti la ulazima kwa taasisi za serikali kufungua akaunti na kuhifadhi mapato na fedha Benki Kuu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti, Hawa Ghasia amepinga kuongezeka ushuru kwa vinywaji baridi akisema hatua hiyo itapunguza uzalishaji.
