Serikali ya Gabon imetangaza kuongeza muda wa kuendelea kwa mazungumzo ya kisiasa nchini humo baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka uliopita.
Mazugumzo hayo ya kitaifa yaliyozinduliwa na rais Ali Bongo , yalitarajiwa kumalizika leo lakini sasa waandalizi wamesema siku ya mwisho ni tarehe 25 mwezi huu.
Imebainika kuwa sababu ya kuahirishwa kuhitimishwa kwa mazungumzo haya ni kuendelea kutafuta mwafaka kuhusu maswala muhimu hasa mabadiliko ya taasisi mbalimbali hususan shughuli za Tume ya Uchaguzi.
Serikali imekuwa ikisema kuwa vyama 50 vya siasa na mashirika ya kiraia vinashiriki katika mazungumzo hayo, ambayo yalisusiwa na mpinzani wake wa karibu Jean Ping aliyedai kushinda Uchaguzi wa mwaka jana.
Mbali na mabadiliko katika Tume ya Uchaguzi, suala lingine linalojadiliwa ni mihula ya rais kuwa madarakani. Kwa sasa rais anahudumu kwa muhula wa miaka saba.
Jean Ping ambaye ameendelea kukataa kumtambua Bongo kama rais wa nchi hiyo, wiki hii alimtumia barua ya pongezi kwa rais mpya wa ufaransa Emmanuel Macron.
