Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) itajenga kiwanda cha viatu kinachomilikiwa na vikosi vya SMZ na mwaka wa fedha 2017-2018 imetenga zaidi ya sh bilioni 1.3.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara maalumu ya vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir amesema maandalizi ya kukiwezesha kiwanda cha kutengeneza viatu na vifaa vya wapiganaji ikiwemo sare yamekamilika.
Amesema maandalizi hayo yamekamilika baada ya Baraza la Mapinduzi kuridhia mpango huo ulioifanya Wizara ya Fedha na Mipango kutenga fedha za ujenzi huo.
Aidha amesema uamuzi wa kujengwa kwa kiwanda hicho unatokana na ushauri wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein kwa vikosi vya ulinzi kuwa na vifaa vya kisasa.
Amesema kamati ya matayarisho ya ujenzi wa kiwanda imefanya ziara katika nchi mbalimbali kujifunza uendeshaji wa kiwanda.
Amevitaja vikosi vitakavyofaidika na ujenzi wa kiwanda hicho kuwa ni Valantia, Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), Kikosi cha Kupambana na Magendo (KMKM), Chuo cha Mafunzo na Idara ya Zimamoto.
