Serikali ya Qatari imeishutumu Saudi Arabia kwa kuvuruga ibada ya Hijja.

Serikali ya Qatari imeishutumu Saudi Arabia kwa kuvuruga ibada ya Hijja ambayo hufanyika kila mwaka katika mji mtakatifu wa Mecca kutokana na hatua yake ya kukataa kuwahakikishia usalama mahujaji wanaoshiriki ibada hiyo.

Saudi Arabia pamoja na washirika wake walikata uhusiano na Qatar tangu Juni 5 mwaka huu wakiishutumu kuyaunga mkono makundi ya itikadi kali na washia nchini Iran.

Mnamo Julai 20 mwaka huu Saudi Arabia ilisema raia wa Qatar wanaotaka kushiriki ibada ya hija ya mwaka huu wataruhusiwa kuingia nchini humo lakini hata hivyo iliweka vizuizi kadhaa.

Wizara inayohusika na masuala ya Hija ya Saudi Arabia imesema mahujaji wa Qatar watakaowasili kwa ndege katika nchi hiyo ya kifalme watapaswa kutumia mashirika ya ndege kwa makubaliano na Saudi Arabia ikiwa ni pamoja na kutakiwa kupata visa pindi watakapowasili mjini Jeddah au Medina sehemu pekee ya mahujaji hao kuwasili nchini humo.

Saudi Arabia pamoja na washirika wake Bahrain, Misri na Umoja wa Falme za kiarabu zilikata mahusiano ya kidiplomasia pamoja na kuiwekea vikwazo Qatar vilivyoendana na kuzuia anga ya nchi hizo kutumiwa na ndege za Qatar.

 

Exit mobile version