Serikali imekitaifisha kiwanda cha kusindika ngozi cha Mwanza Tanneries kilichopo eneo la viwanda Ilemela mkoani Mwanza,baada ya wamiliki wake kushindwa kukiendeleza kuanzia mwaka 1998 hadi sasa,huku ikibaini kuwepo kwa udanganyifu wa umiliki wa kiwanda hicho uliodaiwa kufanywa nakampuni ya Quality group.
Uamuzi huo umetangazwa na mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella mbele ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo,wakiwemo pia wawakilishi wa kampuni ya Caspian na Quality group zilizoshindwa kutekeleza masharti ya mkataba wa kukiendeleza kiwanda hicho.
Kiwanda hicho awali kilikuwa kikimilikiwa na kampuni ya Africa Tanneries kisha kubadilishwa umiliki wake kwenda kwa kampuni ya Kasco ambayo na yenyewe inadaiwa imebadilisha umiliki wake kwa kampuni ya Quality group ambayo inadaiwa imeshindwa kukiendeleza.
Kampuni za quality group na Kasco zimekuwa kwenye mgogoro wa muda mrefu juu ya umiliki wa kiwanda hicho,huku kila mmoja akidai kuwa ndiye mmiliki halali,hadi serikali ilipoamua kukata mzizi wa fitina baada ya kuchukua hatua ya kukifunga na kukitaifisha hadi hapo mwafaka utakapopatikana.
