Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka 2017/18 imetenga Sh18.1 bilioni kwa ajili ya kujenga na kukarabati mahakama mbalimbali nchini.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki alipokuwa akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi(CCM).
Kairuki amesema azma ya Serikali ni kusogeza huduma za mahakama karibu na wananchi na kwamba katika mwaka wa fedha 2016/17 zilitengwa Sh 46.5 bilioni ambazo zimefanya kazi kubwa.
Amesema mahakama ambazo zipo kwenye utaratibu wa kukarabatiwa, ni Mahakama Kuu ya Tanga na Dar es salaam na kuanza ujenzi katika Mahakama Kuu ya Mara na Kigoma.
Katika swali la msingi la Mbunge wa Njombe Mjini (CCM), Edward Mwalongo alitaka kujua kama Serikali itakuwa tayari kukarabati Mahakama za Mwanzo za Mahenye na Igomonyi ili wananchi waweze kupata huduma hiyo karibu.
Akijibu swali hilo Kairuki amesema moja ya changamoto kubwa zinazoikabili Mahakama ni uchakavu wa miundombinu na ukosefu wa majengo ya kutosha.
Amesema mpango uliopo ni kujenga majengo mapya na siyo kukarabati yaliyopo hasa ikizingatiwa kuwa majengo yaliyoombewa na mbunge yapo kwenye hifadhi za barabara na pia ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Njombe ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele.
