Serikali yateua Kamati Maalumu kukagua utendaji wa viwanda.

Serikali imeteua kamati maalumu yenye kushirikisha wataalamu pamoja na wakuu wa mikoa wa kila mkoa, itakayozunguka kukagua utendaji wa viwanda vilivyobinafsishwa, na kisha ndani ya siku 15 itatoa maamuzi.

Imesema viwanda watakavyoshughulika navyo ni vile vilivyobinafsishwa na ambavyo havifanyi kazi, lakini pia kuhakikisha uzalishaji wa kiwanda husika kama ndio ulioruhusiwa.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema hayo jijini Dar es Salaam ,na kuongeza kuwa wapo waliopewa viwanda kwa shilingi moja na wengine kwa Sh. milioni 10, vingine vikifanya kazi, vingine vikiwa havifanyi kazi iliyokusudiwa na vingine kutokufanya kazi kabisa.

Amesema Kamati hiyo itafuatilia na tayari ameandika barua kwa wakuu wote wa mikoa nchini, na kupewa hadidu za rejea ili waweze kupitia kiwanda kimojakimoja kuhakikisha utendaji kazi wake.

Aidha amesema lengo la kubinafsisha viwanda ni ili vizalishe bidhaa ambazo zitatumika nchini na nyingine ziweze kuuzwa nje ya nchi na kuleta fedha za kigeni, vifanye kazi viweze kutoa ajira kwani asilimia 65 ya idadi ya watu nchini n I vijana na wengi wao hawana ajira.

Ametoa wito kwa wakuu wa mikoa, kukagua kiwanda kimoja baada ya kingine na hata kuhoji umiliki, hivyo mhusika anatakiwa kuwa na nyaraka stahiki, kwani ubinafsishaji dhamira yake kubwa ilikuwa ni kuwepo kwa ajira.

 

Exit mobile version