SERIKALI imevunja Bodi ya Baraza la Taifa la Hifadhi ya Usimamizi wa Mazingira (NEMC), sambamba na kufanya mabadiliko ya uongozi huku watumishi wanne wakisimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema hatua hiyo imetokana na kukithiri kwa malalamiko ya wananchi na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Makamba amesema ameamua kutengua uteuzi wa wajumbe wote saba wa Bodi ya NEMC ili baadaye ateuwe wajumbe wapya ambao wataenda na kasi na ari inayohitajika sasa katika kuelekea uchumi wa viwanda.
Hata hivyo amesema Mwenyekiti wa Bodi ambaye mamlaka yake ya uteuzi ni ya Rais, ataendelea kuwepo hadi hapo atakapoteuliwa mwingine na amemteua Dk Elikana Kalumanga, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NEMC hadi hapo rais atakapofanya uteuzi kwa nafasi hiyo.
Kalumunga ni Mhadhiri katika Taasisi ya Usimamizi na Tathmini ya Rasilimali Asili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Waziri Makamba amesema ili kuboresha utendaji wa NEMC, amefanya mabadiliko ya baadhi ya wakurugenzi na wakuu wa kanda, kwa Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa NEMC, Charles Wangwe kumrejesha Wizara ya Fedha na Mipango atakapopangiwa kazi kulingana na mahitaji ya serikali.
Nafasi hiyo itakaimiwa na Adam Minja kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
