Shisha yapigwa marufuku Mkoani Dodoma.

Serikali ya Mkoa wa Dodoma  imepiga marufuku uvutaji wa kilevi aina ya shisha unaoendelea kwenye mahoteli yote mkoani humo, ikisema ni sehemu ya madawa ya kulevya.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa  wa Dodoma JORDAN RUGIMBANA jana  kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani , ambayo yatafanyika leo mjini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa  Waziri Mkuu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzani  KASSIM MAJALIWA.
Mkuu huyo ameongeza kusema  Mkoa wa Dodoma ni mojawapo ya mikoa ambayo imeathirika zaidi na madawa ya kulevya, kwa kuwa ina vijana wengi ambao wapo vyuoni hivyo ni walengwa wakubwa wa madawa hayo.
RUGIMBANA ameeleza kuwa mahoteli mengi yamekuwa na mtindo wa kuweka kilevi aina ya shisha kwa ajili ya kuwavutia wateja wao, na hivyo kukipiga marufuku kilevi hicho mkoani humo.

Naye mwakilishi wa kamishna jenerali wa tume ya kuthibiti madawa ya kulevya ambaye pia ni kamishna msaidizi wa kinga, tiba na utafiti Dk, CASSIAN NYANDINDI, amesema kuwa kuna njia kuu tatu za kupambana na madawa ya kulevya ambazo hutumika duniani kote ambazo ni kuwakamata na kuwathibiti wasambazaji na wauzaji wa dawa za kulevya, kutoa elimu ya madhara ya dawa za kulevya kwa watu ambao bado hawajaingia kwenye matumizi na kutoa fursa ya tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya ili kupunguza madhara yaliyotokana na madawa ya kulevya.

Maadhimisho hayo ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani yatafanyika  kitaifa mkoani Dodoma, ambapo  kauli mbiu   inasema tuwasikilize na kuwashauri vijana na watoto ili kuwaepusha na dawa za kulevya.

 

Exit mobile version