WAZIRI wa nchi ofisi ya Rais (Tamisemi) George Simbachawene amezishauri Halmashauri zilizoko kwenye Mkoa wa Dodoma ,kuitumia Benki ya DCB kupitishia fedha zake za kuwakopesha vijana na wanawake ili fedha hizo ziweze kutumiwa na kurejeshwa kwa wakati.
Simbachawene ametoa kauli hiyo Mjini Dodoma wakati akizindua tawi jipya la benki hiyo, ambalo ni la kwanza kuwa nje ya mkoa wa Dar es Salaam.
Amesema kumekuwa na changamoto nyingi zinazozikabili halmashauri katika urejeshwaji wa fedha, zinazotolewa kwenye vikundi vya vijana na wanawake hivyo akawashauri kuitumia benki hiyo kupitishia fedha hizo, ili ziweze kukopeshwa kwa masharti nafuu na kurejeshwa kwa wakati
Naye mkurugenzi mtendaji wa benki ya DCB, Edmund Mkwawa amesema kuwa benki hiyo imejipanga kukopesha fedha kiasi cha sh. 105 bilion kwa wajasiriamlai na wafanyabiashara wakubwa mkoani Dodoma ambapo katika Wilaya za Mkoa huo,kutakuwa na mawakala zaidi ya 90 ambao watakuwa wanatoa huduma kwa wananchi walioko Wilayani.
