NAIBU Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya amewataka wanafunzi wote nchini, kusoma kwa bidii masomo ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuhakikisha ndoto ya Tanzania ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda na biashara inafanikiwa.
Amesema kuwa sayansi, teknolojia na ubunifu, ndio njia pekee itakayowezesha nchi kupata maendeleo kwa kasi na kupunguza utegemezi wa teknolojia.
Naibu Waziri amesema hayo jana katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani Dar es Salaam wakati wa kukabidhi bendera ya Taifa ,kwa wanafunzi saba wanaosoma masomo ya sayansi wanaokwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ya First Global Challenges nchini Marekani.
Shule zilizotoa wanafunzi watakaoshiriki mashindano hayo ni Jangwani, Benjamin Mkapa, Jamhuri, Feza, Azania na Kisutu ambapo amesema nchi inahitaji viwanda vinavyotumia teknolojia ya kisasa ili kuongeza ufanisi na kwamba roboti zilizoanza kubuniwa na vijana hao ndizo zitakazokuwa msingi wa viwanda hivyo.
Aidha, aliwahimiza wanafunzi wote kutoogopa masomo ya sayansi kwa kuwa ni rahisi na pia kuna uhitaji mkubwa wa wataalamu katika fani mbalimbali.
