Sudan yapokea mualiko kutoka Marekani.

Sudan imepokea mualiko kutoka Marekani wa mafunzo ya pamoja ya kijeshi na Misri, ukiwa ni mualiko wa kwanza wa aina hiyo kwa zaidi ya miongo mitatu.

Mkuu wa jeshi la Sudan, Jenerali Emad al-Din Adawi ametangaza mualiko huo wa mazoezi ya pamoja yajulikanayo kama Bright Star yatakayofanyika nchini Misri, baada ya kukutana na maafisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani wiki hii.

Mkuu huyo wa jeshi la Sudan amesema mkutano wao umefungua mlango kwa mazungumzo zaidi ambayo yanaweza kurejesha tena mahusiano kati ya Marekani na Sudan.

Mnamo mwezi Julai Marekani iliahirisha kwa miezi mitatu uamuzi wake wa kuiondolea vikwazo vya kiuchumi Sudan juu ya rekodi yake ya haki za binadamu na masuala mengine.

Uchumi wa Sudan umeporomoka tangu Sudan Kusini kujitenga mnamo mwaka 2011, na kuondoka na thuluthi tatu ya mafuta yanayozalishwa, chanzo chake kikuu cha fedha za kigeni na mapato ya serikali.

 

 

Exit mobile version