TAASISI isiyo ya Kiserikali ya Hope 4 Young Girls Tanzania imetoa msaada wa baiskeli 60, kwa wanafunzi wa kike wa shule za sekondari za wilaya ya Kisarawe kwa ajili ya kuwasaidia kupunguza tatizo la utoro shuleni kunakotokana na kuishi mbali na shule.
Baiskeli hizo 60 zilikabidhiwa kwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Happiness Seneda katika sherehe za kilele za siku ya kimataifa ya Mtoto wa Afrika ambazo zilifanyika wilayani humo katika kata ya Msimbu .
Akizungumza wakati wa kukabidhi baiskeli hizo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo Salama Kikudo, amesema walifikia uamuzi huo wa kutoa baiskeli hizo kwa wasichana wa Kisarawe baada ya utafiti mdogo waliofanya kuonyesha kuwepo kwa tatizo la utoro na mimba kwa wanafunzi wa kike ambao wanaishi mbali na shule.
Akizungumza katika kilele hicho cha siku ya kimataifa ya Mtoto wa Afrika na mara baada ya kukabidhiwa baiskeli hizo Mkuu wa wilaya aliipongeza taasisi ya Hope4 Young Girls Tanzania kwa msaada huo kwa wanafunzi wa shule za sekondari za kike wilayani kwake.
Kwa upande wake Ofisa Mradi wa ‘Umakini wa Masomo, Urahisi wa Kujifunza’ kutoka Hope 4 Young Girls Tanzania, Winnie Mbowe amesema mradi huo ni endelevu na unalenga kufikia sehemu mbalimbali nchi nzima na kwa kuanzia wameanzia mkoa wa Pwani ambao wameshafika Kibaha na Mkuranga ambako walitoa misaada ya aina mbalimbali.
