Takriban watu wanane wameuwawa katika dhoruba zilizoyakumba maeneo ya pwani ya magharibi hapo jana Jumatano, katika mji wa Cape Town Afrika Kusini, na kuleta mafuriko yaliyosababisha uharibifu mkubwa, pamoja na kulazimisha kufungwa kwa bandari ya Cape Town kwa mujibu wa mamlaka za nchini humo.
Mabadiliko hayo ya hali ya hewa yameharibu majengo, na kupelekea miti kadhaa kuanguka, huku nyumba 46,000 zikibaki bila ya umeme.
Dhoruba hizo pia zimesababisha vurugu katika mifumo ya usafiri baada ya huduma za ndege na reli kukabiliana na upepo na mafuriko.
Moto uliwaka katika maeneo kadhaa kutokana na radi, na kuathiri makaazi ya vibanda ya jamii maskini. Dhoruba hizo pia zimeleta ahueni katika eneo lililokuwa na ukame mkali, na upungufu wa maji tokea mwanzoni mwa mwaka huu.
Mkoa wa Western Cape hata hivyo unasema unahitaji mvua za muda mrefu kutokana na kwamba hifadhi yao ya maji imekuwa ya kiwango cha chini.
