Washambuliaji wa klabu ya Yanga Hamissi Tambwe na Obrey Chirwa, wataikosa mechi yao dhidi ya ya Njombe Mji mwishoni mwa wiki hii mchezo ambao utachezwa katika uwanja wa Saba Saba Njombe.
Wachezaji hao wote walianza mazoezi mepesi jana katika Uwanja wa Uhuru jiji Dar es Salaam chini ya uangalizi maalum wa Daktari, lakini imeonekana hawatakuwa tayari kwa mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Mpaka sasa Tambwe na Chirwa wameondolewa rasmi kwenye Orodha ya kocha Mzambia Geroge Lwandamina, katika mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya wenyeji Njombe Mji Jumapili.
Majeruhi wengine ni kipa Benno Kakolanya na viungo Hussein Akilimali, na Geoffrey Mwashiuya ambao wote tayari wameanza mazoezi mepesi.
Yanga wanatarajiwa kusaka ushindi wa kwanza Jumamosi, katika jitihada za kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu watakapokuwa wageni wa timu iliyopanda Daraja msimu huu
Ikumbukwe mabingwa hao wa Ligi Kuu waliuanza msimu mpya vibaya baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Lipuli ya Iringa iliyopanda Ligi Kuu msimu huu pia.
