TATIZO la jamii kushindwa kutoa ushahidi kwenye kesi zinazohusu ukatili dhidi ya watoto na wanawake ,ni kichocheo cha kutosikilizwa ama kuchelewa kwa kesi hizo na watuhumiwa kutochukuliwa hatua za kisheria.
Hayo yamesemwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Bernad Mpepo wakati wa kikao na watetezi wa haki za binadamu kilichoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za binadamu na jinsia mkoa wa Kilimanjaro (KWIECO).
Amesema kesi nyingi zinachukua muda mrefu na nyingine kufutwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi ,jambo linalonyima haki waathirika wa ukatili huo.
Awali akitoa taarifa kwa wadau wa haki za binadamu wakiwemo Polisi, wanasheria, maofisa ustawi wa jamii na wataalamu wa sheria toka nchini Canada, Mkurugenzi wa Kwieco, Elizabeth Minde alikosoa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971.
Minde aliomba Serikali kufanya marekebisho ya sheria zinazochangia kuongeza matukio ya kikatili ikiwemo sheria hiyo na sheria nyingine kandamizi pamoja na kuwawezesha kitaalamu waendesha mashtaka na maofisa ustawi wa jamii ili kurahisisha utendaji wa upatikanaji wa haki kwa waathirika wa ukatili nchini.
Alisema Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inamtambua mtu mwenye umri wa miaka kuanzia 14 anaweza kuolewa jambo ambalo linakinzana na Katiba ya Tanzania inayomtambua mtu mzima ni kuanzia miaka 18.
Naye mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka shirika la NAFGEM, Francis Selasini alisema ipo haja kwa mahakimu kupewa mafunzo maalumu ya taratibu za kisheria hasa katika kesi zinazohusiana na haki kwa wanawake na watoto, madakta na wauguzi pamoja na maafisa ustawi wa jamii wanaohudumia watoto na wanawake ambao wamekuwa wakifanyiwa vitendo mbalimbali vya kikatili.
