Rais wa Marekani Donald Trump amepuuziia wito wa kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakusitisha vita vya maneno kati ya Marekani na Korea Kaskazini.
Merkel amekosoa mvutano unaoendelea kati ya nchi hizo mbili, akisema kwamba kuendeleza vita vya maneno kati yao si njia sahihi.
Trump amesema kwamba Marekani imejitayarisha na ipo tayari kuchukua hatua za kijeshi iwapo Korea Kaskazini itafanya mashambulizi, amewaambia waandishi habari kwamba kazi ya Merkel ni kuisemea Ujerumani.
Wizara ya mambo ya nje ya China imesema nchi yake ambayo ni mshirika mkuu wa kibiashara kwa Korea Kaskazini, inatarajia pande zote mbili zitachukue jitihada zaidi katika kupunguza mgogoro unaoendelea kwa sasa na kujenga uaminifu wa pamoja, kuliko kuonyeshana nguvu.
Trump atakutana na rais wa China Xi Jinping hapo Ijumaa na watajadili vikwazo vya kisiasa vya ziada dhidi ya taifa hilo ambalo limejitenga na dunia.
