Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa mataifa Stephen O’Brien amekaribisha ahadi ya wahisani ya takribani dola bilioni 6 ili kuisaidia Syria na ukanda mzima kwa mwaka 2017 ikiwa ni ahadi kutoka kwa wahisani 41.
Dola zingine bilioni 3.7 zimeahidiwa na wahisani haohao kwa ajili ya mwaka 2018 na zaidi.
Hata hivyo wakati zahma kubwa kabisa ya kibinadamu na wakimbizi Syria ikiingia mwaka was aba , mustakhbali wa watu na taifa hilo bado uko njia panda ameonya O’Brien.
Umoja wa mataifa na washirika wake waliohudhuria mkutano wa kimataifa wa usaidizi kwa ajili ya Syria mjini Brussels Ubelgiji wanalenga kuwafikia watu milioni 12.8 mwaka huu walio ndani ya Syria na nje kama wakimbizi.
O’Brien amesema mkutano huo kwa ajili ya Syria umemalizika na nia moja ya kimataifa, kuendelea kusaidia mgogoro huo na mamilioni ya watu wanaohitaji msaada.
