Ufaransa imezindua mipango ya kuanzisha vituo vya kusajili wahamiaji wanaotafuta hifadhi huko nchini Libya, huku bara la Ulaya likiwa linakabiliwa na wimbi la wahamiaji wanaovuka bahari ya Mediterenia.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema mpango huo utaanza rasmi msimu huu wa joto na utawapa fursa wahamiaji kutafuta hifadhi wakiwa barani Afrika.
Libya imekuwa kituo kikuu kwa wahamiaji wa Kiafrika wanaojaribu kuingia barani Ulaya kwa kutumia boti dhaifu ambazo mara kwa mara kuzama na zinazoendeshwa na wafanya biashara haramu.
Libya inajaribu kuzuia safari hizo haramu huku yenyewe ikiwa inapambana na ombwe la kitawala na kisiasa tangu kupinduliwa na kuuwawa kwa kiongozi wa zamani na wa muda mrefu Muamar Gaddafi.
