Tume ya Uchaguzi nchini Kenya imemtangaza rais Uhuru Kenyatta kama mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa urais uliofanyika siku ya Jumanne wiki hii.
Baada ya kuhakiki upya kwa fomu zinazoonesha matokeo zilizopewa jina la 34 A na 34 B kutoka maeneo bunge na vituo vya kupigia kura, Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati amesema rais Kenyatta alipata kura Milioni 8.2 sawa na asilimia 54.2 dhidi ya mpinzani wake wa karibu Raila Odinga aliyepata kura Milioni 6.7 sawa na asilimia 44.7.
Ushindi huu unamaana kuwa rais Kenyatta alipata asilimia 50 na kura moja, ya jumla ya kura zilizopigwa lakini pia asilimia 25 ya kura zote angalau katika kaunti 24 kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.
Chebukati ameeeleza kuwa kati ya wapiga kura zaidi ya Milioni 19 waliojiadikisha kupiga kura, Wakenya takriban Milioni 15 walishiriiki katika Uchaguzi huo.
Ushindi wa Kenyatta umekataliwa na muungano wa upinzani NASA na kusema, kura za mgombea wake ziliibiwa na matokeo yalibadilishwa.
Kabla ya kutangazwa kwa mshindi, NASA walikutana na Makamishena wa IEBC na kueleza hoja zao ikiwa ni pamoja na
kutaka wadau wote kuruhusiwa kuthathmini mfumo wa tume hiyo.
Hata hivyo, Mawakala wa Odinga ambao ni Musalia Mudavadi na James Orengo, wamesema madai yao hayajatatuliwa licha ya kuahidiwa na Tume hiyo mapema Ijumaa mchana.
Katiba ya Kenya inaeleza kuwa, yeyote anayekataa matokeo anaweza kwenda Mahakamani lakini, NASA wameonesha kuwa huenda wasiende kulalamikia matokeo haya.
