Umoja wa Ulaya na Uingereza leo zimekamilisha duru nyingine ya mazungumzo ya kibiashara katika hali ya mkwamo huku kila upande ukitoa wito kwa mwingine kubadili mkakati iliyo nao.
Mkuu wa ujumbe wa mazungumzo wa Umoja wa Ulaya Michel Barnier amesema amevunjwa moyo na Uingereza kukosa mwelekeo na kuituhumu serikali ya nchi hiyo kwa kutaka kunufaika na soko la pamoja bila kutimiza wajibu wake.
Barnier pia amezungumzia ukosefu wa mwelekeo kuhusu wajibu wa bunge la ulaya, bunge la Uingereza au asasi za kiraia katika utekelezaji wa mahusiano ya siku za usoni.
Uingereza ilijitoa kutoka Umoja wa Ulaya Januari 31 na pande hizo mbili zina muda wa hadi mwishoni mwa mwaka kukamilisha makubaliano mapya ya kibiashara au kusitisha mazungumzo.
