Ujerumani na China zimeitolea mwito Marekani isiutupilie mbali mkataba wa mabadiliko ya tabia ya nchi ulioafikiwa mjini Paris nchini Ufaransa.
Mwito huo umetolewa kwenye mkutano uliofanyika katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin.
Rais wa Marekani Donald Trump amewahi kusema Marekani itajiondoa kutoka kwa mkataba huo baada ya kusema mabadiliko ya tabia nchi ni uongo.
Ujerumani na China zimeitaka Marekani iuheushimu mkataba huo wa Paris huku Marekani ikijiandaa kuamua mustakabali wake kuhusu mkataba huo.
Katika taarifa ya pamoja mwanzoni mwa Mdahalo kuhusu hali ya hewa huko Petersburg, Berlin, mawaziri wa mazingira wa Ujerumani na China wameitaka Marekani isijiondoe kutoka mkataba wa Paris.
Waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara Hendricks amesema wanawasiliana na maafisa wa ngazi zote za Marekani kuwashawishi wabakie katika mkataba huo.
Hendricks amesema anaamini kubakia kwa Marekani kutaimarisha juhudi za kupunguza ongezeko la joto na huenda kutainufaisha zaidi Marekani kiuchumi.
