Ukosefu wa kituo cha afya katika vijiji vya Kata ya Malolo wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, huwalazimu wananchi kutembea zaidi ya saa nane, kwenda kutibiwa mikoa jirani ya Iringa au Morogoro.
Hali hiyo imedaiwa kuchangia wanawake wengi kujifungulia nyumbani, na hata kupata madhara mbalimbali ukiwamo ugonjwa wa fistula, kutokana na kukaa na uchungu wa uzazi wa muda mrefu.
Diwani wa Kata ya Malolo Maulid Mangile, amesema hali hiyo imekuwa ikiwaathiri zaidi wajawazito hasa wanapougua usiku na watu wengine wanapougua ghafla.
Mangile amesema kutokana na hali hiyo, akinamama wajawazito wamekuwa wakijifungulia njiani na maporini, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao.
