Ummy Mwalimu: Badilisheni Corona Kuwa Fursa Kwa Malezi Ya Familia

Mwandishi wetu, WAMJW                        

Wazazi na walezi nchini wametakiwa kufanya tathimini juu ya fursa na changamoto zilizopo katika familia zao hususani kipindi hiki ambacho jamii inakabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugojwa wa homa kali ya mapafu (COVID-19).
Wito huo umetolewa leo jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akizungumza kuhusu Siku ya Familia Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 15 ya Mwezi Mei.


Waziri Ummy amesisitiza wazazi na walezi kuhakikisha wanatumia kipindi cha mapambano dhidi ya Corona kuwa karibu na familia zao huku wakifanya ufuatiliaji wa karibu hasa kwa watoto na Wazee kwa kufuatilia hali zao za lishe na endapo kuna mabadiliko wachukue hatua stahiki ya kutoa taarifa na kuwapeleka Katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Waziri Ummy ameziasa familia zisiwanyanyapae waliopata maambukizi ya Corona tabia ambayo inaweza kupunguza upendo na utu miongoni mwa Watanzania wakati huu wa mapambano dhidi ya COVID-19.


“Niwaombe wazazi na walezi muwe karibu na familia zenu hasa watoto na wazee na punde mnapobaina dalili za ugonjwa wa Corona watoe taarifa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa” alisema
Amesema wakati wa maadhimisho ya Siku ya Familia wazazi pia wanawajibika kubuni michezo mbalimbali kwa ajili ya watoto ili waendelee kujifunza wakiwa nyumbani itakayokuwa kivutio kwa watoto na hivyo kubaki nyumbani badala ya kuranda mtaani.
Ameongeza kuwa kipindi hiki wakati shule zimefungwa ikiwa ni njia ya kuwaepusha na maambukizi ya virusi vya corona, watoto waandaliwe mazingira bora yatakayowawezesha kuendelea kufuatilia masomo kupitia vyombo vya habari na njia ya mtandao.
 “Familia ni msingi wa ustawi wa Jamii yoyote ile hivyo ni muhimu kuilinda ili kufikia maendeleo endelevu na kuhakikisha tunailinda na maambukizi ya Virusi vya Corona” alisema
Aidha, amesema kutokana na umuhimu wa familia kwa ustawishi wa jamii, Wazazi na walezi wana kila sababu ya kubadilisha tabia, mitazamo na kuongeza maarifa huku wakiongeza mbinu za kuiwezesha familia kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo maambukizi ya Virusi vya Corona.


Amesisitiza umuhimu wa Watanzania kuendelea kufuata kanuni na maelekezo ya wataalam wa afya ili kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 ambayo ni kujiepusha na mikusanyiko, kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji tiririka, kutumia vitakasa mikono kuzingatia umbali wa mita moja na kuendelea kati ya mtu na mtu pamoja na kuvaa barakoa.


 Pia Waziri Ummy amezitaka Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha wanaadhimisha Siku ya Familia Duniani kwa kutoa elimu kwa familia kuhusu namna ya kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona.
Tanzania inaungana na Mataifa mengine ulimwenguni kila tarehe 15 mwezi Mei kuadhimisha Siku ya Familia Duniani ambayo kwa Mwaka huu inaongozwa na Kauli Mbiu isemayo “Familia ni Msingi katika kutokomeza Corona, tuilinde na tuwalinde wengine”
MWISHO.

Exit mobile version