Umoja wa makanisa mbalimbali nchini, unatarajia kufanya maombi ya shukrani kitaifa ya saa tano Jumamosi ijayo.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maombi hayo, Askofu Dk David Mwasota amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi yake jijini Dar es Salaam.
Askofu huyo amesema maombi hayo ni kwa ajili ya kumshukuru Mungu, kwa kuwawezesha kumpata Rais John Magufuli, ambaye amekuwa akiibua na kufichua maovu mbalimbali yaliyokuwa yakitendeka nchini.
Aidha, amesema maombi hayo ni mwitikio wa Rais Magufuli, ambaye mara nyingi amekuwa akisema anahitaji watanzania wamuombee ambapo yatafanyika Julai 15, mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 8 mchana.
Amesema katika maombi hayo, wanategemea kupata ugeni wa maaskofu 17 kutoka Marekani, umoja wa maaskofu wa makanisa Afrika Kusini watakuwepo wajumbe 41 na wajumbe mbalimbali kutoka mikoani hapa nchini ambapo ametoa mwito kwa wakazi wa Dar es Salaam na mikoa jirani, kufika Uwanja wa Uhuru kushiriki.
