Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kusitishwa kwa muda mapigano ili kuruhusu kiasi ya raia 20,000 waliozingirwa kwenye mji wa Raqqa, nchini Syria, waweze kuondoka.
Umoja huo pia umevitaka vikosi vinavyoongozwa na Marekani kusitisha mashambulizi ya anga ambayo yamesababisha majeruhi.
Mshauri wa masuala ya kiutu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Jan Egeland amewaambia waandishi habari mjini Geneva, Uswisi, kwamba boti katika Mto Euphrates hazipaswi kushambuliwa na kwamba watu wanaotoka kwenye boti hizo hawawezi kuhatarisha maisha yao kwa mashambulizi ya anga.
Aidha, mjumbe msaidizi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Ramzy Ezzeldin, amesema umoja huo bado unatathmini matokeo ya mazungumzo yaliyofanyika wiki hii mjini Riyadh kati ya makundi matatu ya upinzani ya Syria ambayo yalishindwa kuungana.
