Urusi imeonya kuwa itashambulia ndege za muungano unaoongozwa na Marekani nchini Syria iwapo ndege hizo zitapaa katika maeneo ambayo jeshi lake linahudumu.
Hii ni baada ya ndege ya kivita ya Marekani kutungua ndege ya kivita ya serikali ya Syria.
Muungano huo unaoongozwa na Marekani ulisema ndege moja yake ilitungua ndege ya Syria aina ya Su-22 baada ya ndege hiyo kuangushia mabomu wapiganaji wanaoungwa mkono na Marekani katika mkoa wa Raqqa, Jumapili.
Urusi, mshirika mkuu wa serikali ya Syria, imesema pia kwamba itakatiza mawasiliano yote na Marekani ambayo lengo lake huwa kuzuia ajali angani.
Syria imeshutumu shambulio hilo la Marekani na kusema litasababisha “matokeo mabaya sana”.
Urusi imekanusha madai kwamba Marekani ilikuwa imewasiliana na maafisa wa urusi kabla ya ndege hiyo aina ya Su-22 kutunguliwa.
