Uturuki leo inaadhimisha mwaka mmoja tangu jaribio la kuipindua serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan mara baada ya kushindwa kufanya mapinduzi hayo.
Tangu jaribio hilo, serikali imeendelea kuwakamata maelfu ya watu wakiwemo wanahabari na kuwafuta kazi maelfu ya wafanyakazi wa umma, maafisa wa usalama, wanajeshi na wasomi.
Serikali itaadhimisha tukio hilo kwa hafla mbali mbali ikiwemo hotuba tatu zitakazotolewa leo na Rais Erdogan katika miji ya Istanbul na Ankara.
Baada ya jaribio hilo la kuipindua serikali ambalo mamia ya watu walikufa, serikali ilitangaza hali ya hatari. Zaidi ya watu 50,000 wako jela kwa kushukiwa kuwa na uhusiano na hasimu mkubwa wa Erdogan, Fethullah Gulen anayeishi uhamishoni Marekani.
Serikali inamtuhumu kwa kupanga mapinduzi hayo, madai ambayo Gulen ameyakanusha.
