Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania, limekemea baadhi ya viongozi wa kidini wanaojipendekeza kwa watu wenye fedha, kwa kutaka kuwaombea ili wapate sadaka nono.
Aidha kanisa hilo limeungana na makanisa ya Uamsho ya Moravian Marekani na duniani kote, kutoa tamko rasmi la kupinga ushoga na usagaji, na kuweka bayana kuwa halitafungisha ndoa za jinsi moja.
Askofu Mkuu wa kanisa hilo Tanzania Emmaus Mwamakula, ameyasema hayo hivi karibuni katika Ibada ya kuwasimika wachungaji, mashemasi na makasisi wa kanisa hilo iliyofanyika katika kanisa la Mbweni Dayosisi Kuu ya Dar es Salaam.
Akizungumza katika ibada hiyo Askofu Mwamakula amesema kuwa, utumishi wa Mungu katika dunia hii umewekwa kwa kusudi la kuleta amani, furaha na umoja katika jamii.
Pia kusaidia waliotindikiwa imani kumkaribia Mungu zaidi na si kujinufaisha wenyewe.
