Waandamanaji wamevamia bunge la Macedonia jana, na kuwashambulia wabunge, akiwemo kiongozi wa upinzani, wakipinga kura ya kumchagua spika mpya.
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Social Democrats Zoran Zaev, alionekana akiwa na damu usoni mwake, huku waziri wa mambo ya ndani Agim Nuhiu akisema wabunge 10 walijeruhiwa, pamoja na baadhi ya askari polisi na waandishi habari.
Vurugu hizo zilizuka baada ya waandamanaji karibu 100 wa kizalendo wanaounga chama hasimu cha VMRO-DPMNE, kuingia bungeni wakipeperusha bendera za Macedonia na kuimba wimbo wa taifa.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, tukio hilo la jana limetokea baada ya chama cha Zaev cha SDSM na wabunge wa asili ya Albania kumchagua spika mpya wa bunge, licha ya spika wa zamani kufunga kikao cha siku.
Spika huyo aliechaguliwa, Talat Xhaferi, ni wa kabila la Albania.
Umoja wa Ulaya ulisema umetiwa matumaini na kuchaguliwa kwa Xhaferi.
