Wachimbaji wadogo wa madini wachuuzi na madalali wa madini nchini, wanatarajia kufanya mdahalo wa kitaifa juu ya umuhimu wa sekta ya madini, na namna ya kuwanufaisha zaidi.
Mkurugenzi wa shirika la Haki Madini Amani Mhinda, akizungumza mji mdogo wa Mirerani, na viongozi wa chama cha wachimbaji madini mkoani Manyara (Marema) amesema mdahalo huo utafanyika mkoani Geita.
Mhinda amesema lengo la mdahalo huo ni kuwaleta wadau mbalimbali, kwa pamoja ili kuzungumzia changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa wachimbaji wadogo, na kutafakari kitaifa maono ya wachimbaji.
Amesema wanatarajia kufanya mdahalo huo mwishoni mwa mwezi Juni, kwa kushirikiana na shirika kiongozi duniani la maendeleo la International Institute for Environment and Development (IIED).
Amesema uchimbaji mdogo wa madini unaweza kutoa mchango chanya,wenye umoja na usawa wa maendeleo endelevu na ukuaji wa uchumi, kwani husaidia mamilioni ya watu hasa wanawake na watoto.
Katibu wa Marema Tawi la Mirerani, Abubakari Madiwa alisema kupitia mdahalo huo wanatarajia wachimbaji mdogo kunufaika kwa kujengewa uwezo
hivyo wamejiandaa kushiriki mara utakapofanyika.
