Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walioshikiliwa mateka waachiwa.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imearifu kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wakishikiliwa mateka na wakimbizi kutoka Sudan Kusini, wameachiwa huru wakiwa salama.
Wafanyakazi hao 16 walikuwa wakishikiliwa na kundi la waasi wa zamani kutoka Sudan Kusini, waliokuwa wafuasi wa makamu wa rais wa zamani wa nchi hiyo Riek Machar, na ambao waliikimbia nchi yao baada ya kuzuka mapigano baina yao ya wanajeshi wa serikali ya Rais Salva Kiir.
Wakimbizi hao walikuwa wakishinikiza kupelekwa katika nchi nyingine, kuepuka msongamano katika kambi ndogo wanakohifadhiwa Mashariki mwa Kongo.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa Wasudan Kusini wapatao milioni tatu wameyapa kisogo maskani yao, wakikimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoripuka mwaka 2013, baada ya Rais Kiir kumfukuza makamu wake, Riek Machar.

Exit mobile version