Wahadhiri wa vyuo vikuu vya serikali nchini Kenya wamesitisha mgomo baada ya serikali kuahidi kuwalipa zaidi mara moja, kulingana na taarifa za jana za viongozi wa muungano wa wahadhiri wa vyuo vikuu nchini humo.
Wanachama wa Muungano wa Vyuo Vikuu UASU walimaliza mgomo wa siku 54 unaohusu malipo mwezi Febuari na kusaini mkataba na serikali mwezi Machi wa ongezeko la malipo la asilimia 17.5 na asilimi 3.9 katika posho za makaazi.
Lakini walianzisha mgomo mpya mwezi huu juu ya utekelezaji wa malipo hayo waliyokubaliana na serikali.
Muungano wa UASU umesema serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 5 mwezi huu za kuwalipa wanachama wa muungano huo na hiyo ndiyo sababu ya kusitisha mgomo wao.
