Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, limeanza kutuma msaada wa kibinaadamu kwa wakimbizi zaidi ya 11,000 kaskazini mwa Angola, ambao wanakimbia ghasia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni moja wamegeuka wakimbizi nchini Congo tangu mapigano yazuke kwenye jimbo la Kasai katikati mwa mwaka jana, huku wengine 25,000 wakivuka kuomba hifadhi nchini Angola.
Msemaji wa UNHCR kusini mwa Afrika, Sharon Cooper, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba ndege ya mizigo ilisafirisha hapo jana shehena ya vyandarua na mablanketi kutokea Dubai.
Uasi wa Kaimuna Nsapu uliozuka katika jimbo la Kasai ya Kati mwezi Agosti mwaka jana umekuwa kitisho kikubwa kwa utawala wa miaka 16 wa Rais Joseph Kabila.
