Wakazi wa mji mdogo wa Merelani wameiomba serikali kuingilia kati vitendo vya unyanyasaji na uzalilishaji vinavyoendelea dhidi ya wafanyakazi katika migodi ya wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite maarufu kama WANA-APOLO , baada ya Mfanyakazi kutoka moja ya migodi hiyo kunusurika kufa baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kuchomwa moto na mwajiri wake.
Wakazi hao wakiongozwa na Diwani wa kata ya Merelani Philemon Oyogo, wameiomba serikali kupitia mamlaka husika kufuatilia mazingira ya kazi wanayopitia wafanyakazi wote katika migodi ya wachimbaji wadogo.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara Francis Masawe amethibitisha kupokea taarifa hizo na kusema tayari wanamshikilia mtu mmoja anayesadikika kuhusika na ukatili huo.
Kwa mujibu wa wenyeji wa eneo hilo wamesema Matukio ya aina hii yamekuwa yakitokea mara kwa mara na kutoa wito kwa serikali na Mamlaka husika kuingilia kati kwa kuchukua hatua stahiki kwa wahusika ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vimeonekana kukithiri katika maeneo haya.
