Wananchi wa Rwanda wanapiga kura hii leo kumchagua Rais na wabunge ambapo wachambuzi wanasema Rais wa sasa Paul Kagame anatarajiwa kupata ushindi mkubwa kwenye uchaguzi huo na kusalia tena madarakani.
Kagame mwenye umri wa miaka 59 anawania nafasi hiyo akishindana na wagombea wengine wawili ambao ni Frank Habineza wa chama cha Democratic Green Party na Philippe Mpayimana ambaye ni mgombea huru.
Washindani hao wa Rais Kagame wamelalmikia kupata muda mdogo wa maandalizi kwa ajili ya kampeni hizo hatua ambayo wakosoaji wa Rais Kagame wanasema ni ushahidi tosha kwa kiongozi huyo kukandamiza upinzani.
Wakati huohuo raia wa Rwanda wanaoishi nje ya nchi walianza kupiga kura hapo jana ikiwa ni siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi huo.
Tume ya uchaguzi ya Rwanda imesema zaidi ya watu Elfu 44,000 waishio nchi za nje walikuwa wakitarajiwa kupiga kura katika vituo 100.
Kagame anawania tena nafasi hiyo baada ya asilimia 98 ya wananchi wa Rwanda kupitisha marekebisho ya katiba kufuatia kura ya maoni iliyofanyika mwaka 2015 ambayo yalimuwezesha kuwania muhula wa tatu wa uongozi.
