Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara mhandisi Zephania Chaula amesema atawachukulia hatua kali za kisheria wanasiasa watakaokwamisha zoezi la upigaji chapa mifugo kwenye wilaya hiyo.
Mhandisi Chaula akizungumza kwenye uzinduzi wa mfumo wa Kitaifa wa utambuzi na ufuatiliaji mifugo katika Kijiji cha Naisinyai alisema utekelezaji huo siyo hiyari au utashi wa mfugaji ni lazima.
Alisema Bunge lilitunga sheria ya utambuzi, usajili na ufuatiliaji wa mifugo namba 12 ya mwaka 2010 na mfugaji asipotekeleza hilo, akipinga au kukwamisha zoezi atapigwa faini ya sh2 milioni au kifungo cha miaka miwili jela.
“Nitawachukulia hatua kali za kisheria wale wote watakaokwamisha zoezi hili ila kwa namna tulivyoanza nimeona mwitikio mkubwa mno,” alisema mhandisi Chaula.
Alisema mfumo huo ni nyenzo muhimu na ya lazima katika ufugaji kwa sasa dunia kote ili kuwezesha kukubalika katika masoko ya kimataifa.
Hata hivyo, akiwapongeza wafugaji wa kata ya Naisinyai wakiongozwa na diwani wao Klempu Kinoka na Mwenyekiti wa kijiji Taiko Laizer kwa kutoa mifugo mingi ipigwe chapa kwenye uzinduzi huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Jackson Sipitieck alisema wanampango wa kuanzisha shamba darasa la mifugo kwa lengo la kuwajengea uwezo wafugaji wa wilaya hiyo.
Sipitieck alisema faida ya chapa ya mifugo kwa wafugaji ni kuweka kumbukumbu za matukio muhimu ikiwemo kuzaliwa, vifo, kupotea, kuhama au kusafirisha chanjo na matibabu mengineyo.
Alisema zoezi hilo litawezesha mifugo ikubalike kwenye masoko ya kimataifa na kukabiliana na usafirishaji holela wa mifugo hivyo kuepuka migogoro.
“Mfumo wa utambuzi na ufuatiliaji wa mifugo tafsiri yake ni utaratibu wa kuwezesha uwepo wa alama na utchangia kuepusha migogoro na wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi,” alisema Sipitieck.
Ofisa mifugo na uvuvi wa halmashauri ya wilaya hiyo Dk Saleh Masaza alisema wanatarajia ng’ombe 437,925 za wilaya hiyo zitapigwa chapa.
Dk Masaza alisema ufuatiliaji wa mifugo na mazao yake katika mnyororo wa thamani ya mifugo uwezekane kupitia mfumo huo na wafugaji wanapaswa kuunga mkono kwa kushiriki ipasavyo katika zoezi hilo.
