Wanawake nchini Iran walizuiwa kuingia uwanja wa taifa wa nchi hiyo, ambapo timu yao ya taifa ilikuwa ikicheza mechi ya kufuzu kombe la dunian dhidi ya Syria, licha ya kuwa na tiketi.
Wanawake hao walikusanyika nje ya uwanja wa Azadi mjini Tehran, kulalamika wakati waliamrishwa kuondoka huku wanawake raia Syria wakiruhusiwa kuingia uwanjani bila tatizo lolote baada ya kuonyesha paspoti zao.
Emeelezwa kuwa wanawake wamepigwa marufuku nchini humo kuhudhuria mechi za kandanda ya wanaume.
Wanawake kadha walikuwa wamenunua tiketi kwa njia ya mtandao, wiki moja mapema kabla ya mechi.
Lakini shiriko la kandanda nchini Iran lilisema kuwa tiketi hizo ziliuzwa kimakosa, na kuahidi kuwarejeshea pesa wanawake ambao walikuwa tayari wamezinunua.
Wale waliokuwa na tiketi hata hivyo waliamua kuelekea uwanjani jana Jumanne wakitaka kujaribu ikiwa wangeruhusiwa kuingia, hata hivyo hawakuruhusiwa.
