Washukiwa 25 wanaodaiwa kupanga njama za mapinduzi wakamatwa Ujerumani

Maelfu ya polisi leo wamefanya msururu wa misako kote Ujerumani wa washukiwa wa siasa kali za mrengo wa kulia wanaodaiwa kupanga njama ya kuipindua serikali kwa kutumia silaha. Waendesha mashitaka wa serikali wamesema karibu maafisa 3,000 walifanya misako hiyo ya kile kinachofahamika kama vuguvugu la Reich Citizens.

Baadhi ya wanachama wa kundi hilo wanapinga katiba ya Ujerumani iliyoandikwa baada ya vita na wametoa mwito wa kuangushwa kwa serikali. Waendesha mashitaka wanasema raia 22 wa Ujerumani wamekamatwa kwa kushukiwa kuwa waanachama wa kundi la kigaidi. Watu wengine watatu, akiwemo raia wa Urusi, wanatuhumiwa kuliunga mkono kundi hilo.

Jarida la kila wiki la Der Spiegel limeripoti kuwa maeneo yaliyofanyiwa msako yanajumuisha kambi ya kitengo maalum cha vikosi vya Ujerumani KSK katika mji wa kusini magharibi wa Calw. KSK katika siku za nyuma ilituhumiwa kwa madai kuwa baadhi ya wanajeshi wake wanajihusisha na siasa kali za mrengo wa kulia.

Exit mobile version