WATU 20 wamekamatwa kwa kukutwa na shehena ya bangi gunia 168 katika kitongoji cha Engendeko, Kijiji cha Losinoni wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Akithibitisha kukamatwa kwa shehena hiyo ya bangi Kamishna wa Intelijensia wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Fredrick Kibute amesema ofisi yake ilishirikiana na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kutoka Oljoro ili kufanikisha kazi hiyo.
Aisha amesema kuwa walipata taarifa kutoka kwa raia wema na wiki iliyopita tukatuma kikosi maalumu, kwa ajili ya uchunguzi na baada ya kupata taarifa za uwepo wa bangi hiyo na kupanga safu ya kikosi kazi kwa ajili ya kuja Arusha kukamata bangi hiyo ambayo awali wananchi hao waligomea uongozi wa wilaya baada ya kutakiwa kukisalimisha.
Kamishina Kibute ametumia fursa hiyo kuwaonya wananchi wa Wilaya ya Arumeru kuacha mara moja tabia hiyo ya kulima bangi, na kuwataka wasome alama za nyakati badala ya kufanya kilimo hicho kwa mazoea.
Serikali ya Wilaya ya Arumeru tangu Agosti mwaka jana ilianza kupambana na kudhibiti kilimo cha bangi katika kata 14 na vijiji 22, ambavyo vilikuwa vinategemea kilimo cha bangi kama kitega uchumi cha kujipatia kipato.
